Mahojiano ya kusaka mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi na uratibu wa mipaka IEBC yameingia siku ya pili hii leo.
Erastus Edung Ethekon amekua wa kwanza kufika mbele ya kamati ya uteuzi.
Wengine wanaohojiwa hii leo ni pamoja na aliyekuwa Karani wa Jiji la Nairobi Jacob Ngwele, mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya kusambaza umeme nchini, Kenya Power, Joy Masinde Mdivo na Francis Kaikai Kissinger
Akizungumza alipofika mbele ya kamati ya uteuzi inayoongozwa na wakili Nelson Makanda, Edung amesema vijana, husasan kizazi cha Gen- Z, watakuwa na usemi katika mustakabali wa taifa iwapo watajumuishwa kikamilifu katika uchaguzi wa mwaka wa 2027.
“Vijana hawa wamekua kimya kwa muda lakini sasa tunaona wanaanza kupaza sauti nitapea kipaumbele uhamasisho kuhakikisha wanajisajili na kujitokeza kupiga kura.” Amesema Edung.
Edung pia amependekeza matumizi ya mitandao ya kijamii kufikia vijana.
“Iwapo nitateuliwa kama mwenyekiti nitatafuta mbinu ya kufikia vijana hawa popote waliko na kwa lugha wanayoelewa Zaidi iwe ni katika tiktok, X , ama Instagram lazma tutawafikia.”Ameongeza Edung.
Hapo jana aliyekuwa msajili wa mahakama Anne Amadi, aliyekua mwenyekiti wa tume ya utekelezaji wa Katiba, CIC, Charles Nyachae, Hakimu Abduqadi Lorot na Edward Katama walihojiwa na kamati hiyo.