Baraza la magavana linawataka wahudumu wa afya wanaogoma kusitisha mgomo na kurejea kazini wakati huu taifa linapambana na janga la corona.
Mwenyekiti wa baraza hilo aliyepia gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya badala yake amewataka wahudumu wanaogoma kusuluhisha malalamishi yao na kaunti husika.
Oparanya katika taarifa anasema kwa sasa serikali za kaunti zinakumbwa changamoto za kifedha kwani hazijapokea pesa za Octoba, Novemba na sasa Disemba hali ambayo imefanya vigumu kwa shughuli za kawaida kuendelea.
Amesema imekuwa vigumu kulipa hata mishahara ya wafanyikazi kwa hivyo kuwataka wahudumu wa afya kuelewa hali hiyo na kurejea kazini.
Mgomo huo wa wauguzi na maafisa wa kliniki umeingia siku ya nne huku huduma za matibabu katika hospitali za umma kote nchini zikiathirika.
Wahudumu hao wa Afya wanaogoma wanasema hawana mipango ya kurejea kazini licha ya mahangaiko wakenya wanapitia hadi pale matakwa yao yatakapotimizwa.
Wakati uo huo
Viongozi wa miungano ya wahudumu wa afya imezitaka serikali za kaunti kukoma kuwatishia wahudumu wa afya wanaogoma.
George Gibore, katibu mkuu wa muungano wa matabibu KUCO amewataka wanachama wake kusalia kwenye mgomo na wasiogope vitisho kutoka kwa serikali za kaunti.