Baraza la magavana (CoG) limelalamikia kuathirika pakubwa kwa shughuli za utoaji huduma katika serikali za kaunti kufuatia utata unaozingira mswada wa ugavi wa mapato katika serikali za magatuzi.
Kupitia taarifa, CoG chini ya uongozi wake gavana wa Kakamega Wycliffe Ambetsa Oparanya limesema mgogoro huo umefanya vigumu kwa serikali za kaunti kukosa pesa kulipia mishahara ya wafanyikazi wake na zaidi kutatiza oparesheni za kila siku.
Mgogoro huo unaendelea kushuhudiwa licha ya kubuniwa kwa kamati ya watu 12 kutanzua kitendawili hicho, ripoti zikiarifu kwamba wanachama wa kamati hiyo wameshindwa kuelewana.
Baraza hilo vile vile linatoa wito kwa sekta ya uchukuzi wa umma kutolegeza masharti ya kuzuia msambao wa virusi vya corona baada ya kubainika kuwa magari mengi ya uchukuzi wa umma yamerejelea hali ya kawaida.