Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) imetoa tahadhari kwa madereva kutokana na mvua kubwa inayonyesha kwa sasa kote nchini.
Kwenye notisi yake, NTSA imewataka madereva kuwa ange na kutoingia kwenye madimbwi ya maji yaliyokusanyika barabarani.
“Huenda vidimbiwi vikawa na upana na urefu usiokadirika kwa kutazama kwa macho” NTSA imesema
Nairobi na maeneo mengine kadhaa ya nchi yalianza kupokea mvua jana jioni na yanatarajiwa kuzidi kupokea mvua mpaka alasiri ya kesho.
Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya inatabiri kuwa mvua kubwa itaendelea kunyesha hadi Jumanne, Machi 11, huku mvua ikitarajiwa kuzidi mwa milimita 20 katika muda wa saa 24.
Maeneo yanayotarajiwa kupokea mvua ni Nairobi, Kericho, Bomet, Homa Bay, Siaya, Migori, Busia, Kisumu, Kisii, Nyamira, Nandi, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Baringo, Nakuru, Trans-Nzoia, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet na Pokot Magharibi.
Madereva wametakiwa kuchukua tahadhari kwani Ukungu huenda ukakolea katika baadhi ya barabara hali ambayo huenda ikapunguza uwezo wa kuona mbali.