Machifu watano waliotekwa nyara na kundi haramu la Al-Shabaab mwezi Februari katika kaunti ya Mandera hatimaye wamewachiliwa huru.
Machifu hao walipelekwa Somalia mara tu baada ya kutekwa tarehe 17 Mwezi huo wa Februari.
Watano hao waliwachiliwa Jumapili jioni kufuatia kile mamlaka za eneo hilo imesema ni mazungumzo kati ya wazee wa jamii hiyo na wanamgambo hao wa Al-Shabaab .
Machifu hao walikua safarini kuelekea kwenye mkutano kujadili ulinzi wa Rais William Ruto wakati wa ziara yake katika kaunti hiyo wakati walitekwa.
Wakati wa ziara hiyo, Rais aliahidi kukabili ugaidi haswa katika mpaka wa Kenya na taifa jirani la Somalia.