Mabadiliko serikalini: Rais Ruto awahamisha makatibu na kufanya teuzi mpya.

0

Rais William Ruto amefanya mabadiliko ya makatibu wa wizara mbalimbali kwenye serikali yake kwa kuwateua wapya na kuwahamishia wengine kwenye idara mbalimbali za serikali.

Kupitia taarifa iliyotiwa saini na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, mabadiliko hayo yanatokana na hitaji la kutumia fursa ndani ya sekta zinazoibukia za uchumi.

“Kwa pamoja, mabadiliko hayo yanalenga kurahisisha zaidi utekelezaji wa mwongozo wa kiuchumi wa kijamii wa utawala uliopo na ajenda ya Bottom up” taarifa hiyo ilieleza.

Katika mabadiliko hayo, aliyekuwa katibu wa afya Harry Kimtai amehamishiwa katika idara ya uchimbaji madini, Bellio Kipsang akihamishiwa idara ya uhamiaji, na nafasi yake ya elimu ya msingi ikipewa Julius Bitok aliyeshikilia idara ya uhamiaji.

Amos Gathecha, aliyekuwa katibu katika wizara ya huduma za umma, amepandishwa cheo na kuwa naibu mkuu wa utumishi wa umma chini ya Felix Koskei.

Prof. Edward Kisiangani ambaye amekuwa katibu katika idara ya utangazaji ambaye ameonekana kujipata katika mzozo na wamilki wa vyombo vya habari kutokana na maamuzi ya idara hiyo amehamishwa na kufanywa mshauri mkuu kwenye baraza la washauri wa rais kwenye masuala ya uchumi.

Wakati huo huo kiongozi wa taifa amewateuwa makatibu kumi na wanne wapya miongoni mwao Jane Kare Imbunya ambaye ameteuliwa kuhudumu katika idara ya huduma za umma, Regina Akoth Ombam idara ya biashara, Cyrell Wagunda Odede idara ya uwekezaji naye Caroline Wanjiku Karugu aliyekuwa kwenye kikosi cha kampeni ya Raila Odinga aliposaka uwenyekii wa AUC akiteuliwa kuhudumu katika idara ya maslahi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aliyekuwa katibu wa muungano wa madaktari (KMPDU) daktari Ouma Oluga ameteuliwa kuwa katibu katika idara ya huduma za matibabu kuchukua mahali pa Harry Kimtai huku Ahmed Ibrahim akiteuliwa kuhudumu katika idara ya mipango ya serikali kwenye ofisi ya waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi.

Judith Pareno ambaye amekuwa mwanachama wa muda mrefu wa ODM amepewa idara ya haki na masuala ya katiba.

Waziri wa zamani wa afya Susan Nakhumicha amefanywa mwakilishi wa kudumu kwenye shirika la mazingira la umoja wa mataifa (UN Habitat) hapa jijini Nairobi.

Kiongozi wa taifa pia amewateuwa watu mbalimbali kuwa wakilishi katika mataifa ya kigeni.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here