Maafisa wote wa polisi ambao wako likizoni waliamriwa Jumatano kurejea kazini mara moja.
Maafisa hao Wanatakiwa kuimarisha usalama wakati ambapo msimu wa Krismasi na mwaka mpya Unapodogea.
Katibu katika Wizara ya Mambo ya Ndani Dkt Raymond Omollo amesema Kamati zote za Usalama na Ujasusi za Mikoa na Kaunti zimeagizwa kuendesha vituo vya kusimamia usalama vitakavyokua na maafisa kutoka mashirika yote ya usalama.
“Vituo vyote vya kusimamia usalama vitasimamiwa kwa saa 24, siku saba kwa wiki. Huduma ya Polisi ya Kitaifa itatayarisha Amri za Operesheni za msimu wa sherehe ili kuratibu shughuli za usalama katika kaunti zote,” amesema Omolo.
Maeneo yote manane ya taifa yatakua na vituo vyao, huku kila kaunti ikiwa na Kituo chake maalum huku oparesheni zote zikisimamia na kituo cha kitaifa kitachokuwa kwenye kambi la jeshi la Langata jijini Nairobi.
Oparesheni hiyo itajumuisha maafisa kutoka Jeshi la Ulinzi la Kenya KDF, Huduma ya Kitaifa ya Polisi NPS, maafisa wa Magereza KPS, Huduma ya Wanyamapori KWS na Huduma ya Misitu ya Kenya KFS .
Wakenya pia wanapaswa kutarajia kuona uwepo zaidi wa maafisa wa polisi kutoka vitengo maalum ikiwa ni pamoja na Kitengo cha Timu ya Silaha na Mbinu Maalum (SWAT) na Maafisa wanaovalia nguo za raia.
“Kundi hilo litaimarisha doria na kuongeza ufuatiliaji katika miji mikubwa, maeneo ya ibada na maeneo muhimu ya miundombinu,” Omolo amedokeza.
Ameongeza kuwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi kwa ushirikiano na Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA) itahakikisha utiifu wa sheria za trafiki kupunguza visa vya ajali barabarani.