Tume ya kitaifa ya huduma ya polisi (NPSC) imetangaza kupandishwa vyeo kwa maafisa 738 wa polisi.
Katika taarifa yake ya Jumatano mwenyekiti wa tume hiyo Eliud Kinuthia amesema kuwa baada ya kudurusu mapendekezo kutoka kwa inspekta jenerali wa polisi Douglas Kanja, tume hiyo iliridhia kuwa maafisa hao walikuwa wanastahiki kupandishwa vyeo.
Ni mapendekezo ambayo tume hiyo imebainisha kuyapokea kulingana na sharia wakati wa mkutano wake uliofanyika tarehe kumi mwezi wa Machi mwaka wa 2025.
“Inspekta jenerali aliihakikishia tume kuwa mchakato huo ulikuwa wenye ushindani na uwazi uliozingatia usawa wa maeneo na jinsia kabla ya kuwateua wahusika kuambatana na kipengele cha 10 na 232 kuhusu maadili ya kitaifa ya kanuni za uongozi na huduma ya umma.” Alisema Kinuthia.
“Sawia, kuambatana na kipengele cha 246 (a), tume iliafikia uamuzi wa kuwapandisha vyeo maafisa 738 wa polisi katika vitengo vya huduma ya Kenya Police, huduma ya polisi wa utawala, na idara ya upelelezi,” taarifa ya inspekta jenerali iliongeza.
Maafisa waliopandishwa vyeo wanajumuisha 14 watakaohudumu katika ngazi ya wasaidizi wakuu wa inspekta jenerali wa polisi (SAIG), 51 waliopandishwa kwenye cheo cha msaidizi wa inspekta jenerali wa polisi (AIG), 135 watakaohudumu katika nafasi ya makamishna wa polisi (CP), 277 wamepandishwa hadi ngazi ya wasimamizi wakuu wa polisi (SSP) na 261 kuwa wasimamizi wa polisi (SP).
Wakati huohuo jumla ya wafanyikazi 50 wa huduma ya kitaifa ya polisi wasio maafisa wa polisi na wanaohudumu katika idara mbalimbali waliweza kupandishwa vyeo.
NPSC imedokeza kwamba waliopandishwa vyeo na ambao tayari wameorodheshwa katika gazeti rasmi la serikali ni kati ya walioshiriki mahojiano yaliyoandaliwa mwezi Oktoba mwaka wa 2024.