KITUO CHA POLISI, MAGARI YA POLISI YACHOMWA MAANDAMANO YAKISHUHUDIWA MAJENGO, PUMWANI

0

Maandamano yaliyosababishwa na mauaji ya vijana wawili mtaani Pumwani yamechukua mkondo mwingine kufuatia kuteketekezwa kwa kituo cha Polisi cha Shauri Moyo.

Magari mawili ya polisi na afisi za chifu sawia zinaripotiwa kuteketezwa na wenyeji wenye ghadhabu wakati wa Maandamano hayo mtaani Pumwani na Shauri Moyo, Nairobi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi jijini Nairobi George Sedah, vijana hao mmoja wao akiwa mwenye umri wa miaka 17 wanaripotiwa kupigwa risasi na afisa wa polisi aliyekuwa akiendesha oparesheni dhidi ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Hata hivyo wenyeji wamelalama kuwa afisa huyo alikuwa akichukua hongo kutoka kwa walanguzi.

Ripoti kutoka vituo vya kutetea haki za kijamii zimefichua kuwa watu watatu zaidi wameripotiwa kujeruhiwa huku maafisa wa polisi wakiendelea na juhudi za kuwatawanya umati wa watu wenye ghasia.

Ghasia hizo zinakuja wakati ambapo Kenya tayari inakabiliana na mauaji yanayoshukiwa kuwa ya kiholela.

Katika taarifa hapo jana , Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNCHR) iliibua wasi wasi kuhusu ripoti za wenyeji kuteswa na polisi, utekaji nyara na hata mauaji katika misheni ya ‘Ondoa Jangili’ inayoendelea katika kaunti za Isiolo na Marsabit.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here