Uchunguzi wa mauaji ya mwanaharakati na mwanasiasa kutoka Molo kaunti ya Nakuru Richard Otieno umekabidhiwa kitengo cha mauaji katika idara ya upelelezi wa makosa ya Jinai DCI
Timu ya wapelelezi wa mauaji kutoka makao makuu ya DCI tayari wamejiunga na uchunguzi unaonuia kutegua kitendawili cha mauaji ya Otieno.
Otieno alipatikana Jumamosi, Januari 18 akiwa amefariki Elburgon, Molo, Kaunti ya Nakuru.
Timu inayoongozwa na Mkurugenzi wa Mauaji Martin Nyuguto Jumanne ilitembelea eneo la uhalifu ambapo Otieno alipigwa kwa shoka hadi kufa na watu wasiojulikana.
Baadaye wapelelezi hao walifanya kikao na familia ya Otieno ambapo waliihakikishia uchunguzi wa kina na kuhakikisha haki kwa mpendwa wao.
Nyuguto ameahidi kuhakikisha kuwa waliotekeleza mauaji hayo ya kinyama wanalipia matendo yao.
Otieno aliripotiwa kuuwawa nje ya lango lake baada ya kutazama mechi katika baa moja ya eneo hilo, polisi na wenyeji walisema.
Mauaji hayo yalisababisha maandamano eneo la Elburgon ambapo waandamanaji walitoa mwili wa Otieno kwenye makafani na kuupeleka kwenye kituo cha polisi cha Elburgon kabla ya kufululiza nao hadi nyumbani kwa mbunge wao Kimani Kuria.