Naibu Rais Kithure Kindiki amempongeza Rais William Ruto kwa kufanya kazi kwa pamoja na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, ambao hapo awali walikuwa wakihasimiana.
Akizungumza wakati wa sherehe za Jamhuri, Kindiki amesema maelewano kati ya viongozi hao itachochea maendeleo humu nchini.
“Tunakupongeza kwa kuwasiliana na Waziri Mkuu wa zamani kwa ajili ya kuanzishwa kwa serikali pana, na kwa kuwasiliana na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, na kuhakikisha kwamba kwenda mbele, kila mdau yuko mezani tunapoamua hatima ya nchi yetu kwa heshima ya kizazi kilichopita na vizazi vijavyo,” amesema Kindiki.
“Tunakupongeza kwa kutambua kwamba maendeleo ya Kenya yatakuwa ya haraka ikiwa nchi itaungana. Asante kwa kuwafikia wadau wengi iwezekanavyo ili kuleta kila mtu mezani ili sote tuvute upande mmoja.” Ameongeza Naibu wa Rais.
Jumatatu wiki hii , Rais Ruto alimtembelea Rais Kenyatta nyumbani kwake Gatundu kwa kile alichokiita majadiliano yaliyojikita katika kukuza umoja wa kitaifa na kushughulikia migawanyiko ya kikabila nchini Kenya.
Kenyatta alikataa kuunga mkono azma ya Ruto ya kugombea urais mwaka 2022, badala yake akaweka uzito wake nyuma ya Odinga kama mrithi wake.
Odinga alipoteza kiti cha urais kwa Ruto katika kinyang’anyiro cha Agosti 2022 ambacho matokeo yake aliyapinga mahakamani bila mafanikio.
Rais Ruto tayari yuko kwenye maelewano na Odinga chini ya mpango wa ‘Broadbased Government’ ambapo wandani wa Odinga wameteuliwa kwenye baraza la mawaziri.
Kuna tetesi kuwa kufuatia mkutano wa Siku ya Jumatatu huenda wandani wa Kenyatta sawia wakapata viti kwenye baraza la mawaziri na kwenye nyadhfa kuu serikalini.