Watu wawili wamefariki baada ya upepo mkali uliotokana na kimbunga cha Tropiki IALY kukumba maeneo mbalimbali ya pwani ya Kenya siku ya Jumanne.
Miongoni mwa walioaga ni Mwanafunzi mwenye umri wa miaka minne aliyepoteza maisha baada ya upepo mkali kupiga Shule ya chekechea ya Msikiti wa Gogoraruhe mwendo wa saa kumi jioni na kuharibu paa.
Polisi wamesema kuwa mwanafunzi huyo aliaga alipokuwa akipelekwa hospitalini; wanafunzi wengine watano wanaendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Mariakani
Wanafunzi hao wenye umri wa miaka mitano, miwili na wawili kati yao wakiwa na miaka minne wanauguza majeraha mabaya kichwani baada ya kuangukiwa na paa.
Mkuu wa polisi eneo la Pwani George Sedah amesema mali ya thamani isiyojulikana iliharibiwa katika machafuko yaliyofuata huku upepo ukivuma katika eneo hilo.
“Tumetuma timu kupeleleza vijijini na kutoa taarifa viwango vya uharibifu uliyosababishwa na janga hili, ,” amesema Sedah.
Kifo cha pili kilitokea katika eneo la Watamu ambapo jamaa mmoja aliaga baada ya kuangukiwa na paa ya chumba chake.
Idara ya Utabiri wa Hali ya anga imeonya wavuvi dhidi ya kuelekea baharani mkurengezi wa Idara hio David Gikungu akisema upepo unatarajiwa kuendelea kuvuma.