Bunge la kitaifa litakuwa na wabunge 360 waliochaguliwa, wabunge 6 wa kuteuliwa huku bunge la Senate likiwa na Maseneta 94.
Haya ndio baadhi ya mapendekezo kwenye mswada wa BBI ambayo inapendekeza kila kaunti kumchagua mwanamume na mwanamke.
Kaunti ya Nairobi itakuwa na maeneo bunge mapya 12, Kiambu 6, Nakuru 5 na Kilifi 4.
Mombasa, Kwale, Machakos, Bungoma na Uasin Gishu yataongezewa maneo bunge mapya 3 kila mmoja.
Rais Uhuru Kenyatta na ndugu yake Raila Odinga wakiongoza shughuli ya kukusanya sahihi za mswada huo wa marekebisho ya katiba wamewasihi Wakenya kujitokeza kwa wingi kutia saini zao ili kufanikisha marekebesho hayo wanayosema yatatoa mwanzo mpya kwa taifa hili.
Kwa upande wake, Odinga amesema kupitia kwa BBI, wakenya wataweza kuafikia malengo ambayo taifa limetamani kwa muda mrefu.
Kutakuwepo na nafasi ya kiongozi rasmi wa upinzani ambaye ataibuka wa pili katika uchaguzi wa urais, wadhifa wa waziri mkuu ambaye atateuliwa na rais na manaibu wake wawili utarejeshwa.
Waziri mkuu ataidhinishwa na bunge kabla ya kuapishwa.
Mswada huo pia unalipa bunge la Senate mamlaka zaidi kumulika ugatuzi ikiwemo matumizi ya rasilimali katika serikali za kaunti.
Aidha, kutabuniwa afisi ya Ombudsman kupokea malalamishi kuhusu utendakazi wa idara ya mahakama kibarua cha kumteua atakayeshikilia wadhifa huo kikipewa rais na kisha kuidhinishwa na bunge la Senate.
Kuhusu maendeleo mashinani, kutubanuniwa hazina ya ustawishaji wadi itakayosimamia na MCA kuongezea kwa CDF inayosimamiwa na wabunge.
Tume ya vijana itasalia kuwepo kushughulikia maslahi ya vijana huku makamishna wa tume ya kuratibu mishahara ya watumishi wa umma wakihudumu kwa muda usiokamilka.