KANISA LA KIANGLIKANA LAAGIZWA KUMREJESHEA RAIS RUTO MCHANGO ALIOTOA KWA KANISA BUNGOMA

0

Ufa Kati ya Serikali ya Rais William Ruto na makanisa Unaonekana kuongezeka Askofu Jackson Sapit wa kanisa la Kianglikana sasa akifuata mkondo wa maaskofu wa Kanisa katoliki wa kukataa michango kutoka kwa Rais na wanasiasa wengine.

Sapit ameagiza mchango wa shilingi milioni tano uliotolewa na Rais William Ruto kupitia Gavana wa Bungoma Ken Lusaka kurejeshwa mara moja kwa Rais akisema haukutolewa kwa nia njema.

“Kilichofanyika Bungoma kilikua cha Kusikitisha. Kilikuwa ni kama Kujaribu kuona kanisa la Kianglikana kitafanya nini kufuatia hatua ya Kanisa Katoliki kukataa michango ya Rais.” Amesema Sapit kwenye kikao na wanahabari.

“Hatuta ruhusu Tamaduni nzuri ya matoleo kanisani itekwe nyara na watu wenye maslahi ya kibanfsi” Askofu huyo ameongeza.

Kanisa Katoliki kupitia kwa Askofu wa Jimbo la Nairobi Phillip Anyolo liliagiza zaidi ya shilingi milioni 7 zilizotolewa na Rais William Ruto na Gavana wa Nairobi Jackson Sakaja kurejeshewa viongozi hao.

Anyolo alisema kuwa michango kutoka kwa wanasiasa iliharamishwa na uongozi wa kanisa hilo nchini.

Sapit ameongeza kuwa uozo wa ufisadi umekolea katika miamala yote ya serikali na kwenye utumishi wa umaa.

“Kila sehemu ya Serikali kuanzia Bunge, Mahakama hadi idara tendaji imehusishwa na ufisadi. Hata Tume na afisi huru sawia zimehusishwa na ufisadi.” Amesema Sapit.

Sapit ni miongoni mwa viongozi wa kidini ambao hapo awali walionekana kukumbatia utawala wa sasa ulipoingia madarakani.

Sapit amesema kuwa kanisa la ACK na makanisa mengine chini ya mwavuli wa NCCK yataendelea kuwazuia wanasiasa kuhutubia waumini maabadani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here