Waziri wa Afya Aden Duale amezindua rasmi kamati itakayokagua madeni ya bima ya zamani ya afya (NHIF).
Kamati hiyo iliyozinduliwa Jumatatu ina jukumu la kukagua madeni ambayo hospitali mbalimbali zinadai serikali baada ya kutoa huduma chini ya bima ya NHIF.
Katika kubaini uhalali wa madeni kamati hiyo sawia itahitajika kukagua visa vinavyohusha hospitali zilizotoa huduma za matibabu bila kandarasi halali, madeni yaliyozidishwa, miongoni mwa masuala mengine.
Kamati hiyo inayoongozwa na mwenyekiti James Ojee imetwikwa jukumu la kukagua madeni hayo kuanzia Julai 1, 2022 hadi Septemba 30, 2024, kisha kuishauri wizara ya Afya.
Wanachama wengine wa kamati hiyo itakayohudumu kwa muda wa miezi 3 ni pamoja na; Anne Wamae (makamu mwenyekiti), Edward Bitok, Meshack Matengo, Meboh Awour, Tom Nyakaba, Catherine Bosire, Paul Wafula, Catherine Mungania, James Oundo, Jackline Njiru, Judith Awinja na David Dawe.
Waziri Duale ameitaka kamati hiyo kutoshawishiwa na yeyote wakati wa utendakazi wake.
“Baini na mpendekeze hatua hitajika kuhusu madeni yoyote yasiyokuwa halali, baini visa vyovyote vya vinavyohusisha ufisadi na ripoti za matibabu zisizo za kweli na mtoe mapendekezo faafu kwa idara husika za serikali.” Waziri Duale aliitaka kamati hiyo.
Kulingana na wizara ya afya, rekodi zilizopo zinaonyesha kuwa NHIF inadaiwa takriban shilingi bilioni 33 na hospitali baada ya kutoa huduma za matibabu chini ya bima hiyo.
Kamati hiyo ilibuniwa baada ya rais William Ruto kuagiza kuwa madeni yaliyozidi shilingi milioni kumi yakaguliwe ndani ya kipindi cha siku tisini ili kubaini uhalali wake kabla ya kulipwa.