Mshindi wa medali ya fedha katika urushaji wa mkuki katika Olimpiki ya mwaka 2016 Julius Yego analenga kutinga hatua ya tatu bora kwenye Ligi ya Diamond ya Zurich Septemba tarehe tano 2024.
Yego amebainisha kuwa kumaliza katika ngazi ya tatu bora itamhakikishia alama za kutosha kumpeleka kwenye fainali ya Brussels mnamo Septemba 13-14.
Mashindano ya urushaji mkuki yanajumuisha mikutano mitano-Doha, Paris, Lausanne, Zurich na Brussels. Ni sita pekee kutoka kwa wanne wa kwanza ndio wanaofuzu kwa fainali huko Brussels. Mwanariadha huyo maarufu kama The-YouTube-Man, Mwana Olimpiki mara tatu, yuko katika nafasi ya 10 kwenye viwango vya ubora akiwa na alama nne – alama moja baada ya kumaliza katika nafasi ya nane mjini Doha na alama tatu baada ya kumaliza katika nafasi ya sita mjini Lausanne mwezi uliopita.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 bado anajiamini. Washindi katika kila mkondo wanapata alama nane huku nafasi ya pili na ya tatu wakipata alama saba na sita mtawalia.
Anderson Peters wa Grenada na Jakub Vadlejch wa Jamhuri ya Czech tayari wamepata nafasi zao mjini Brussels.
Peters anaongoza kundi hilo akiwa na alama 21, tano mbele ya Vadlejch. Mshindi wa medali ya fedha ya Olimpiki Neeraj Chopra wa India ni wa tatu kwa alama 14 sawa na Julian Weber wa Ujerumani.
Arthur Felfner wa Ukraine anashika nafasi ya tano akiwa na pointi tisa, Andrian Mardare wa Moldova (wa sita akiwa na pointi nane) na Roderick Genki Dean wa Japan (wa saba na pointi sita).