Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja amekana madai kuwa Mbunge wa zamani wa Limuru Peter Mwathi ametiwa mbaroni kufuatia vurugu ilIyoshuhudiwa jana kwenye hafla ya mazishi iliyohudhuriwa na Naibu wa Rais wa zamani Rigathi Gachagua.
Kanja amesema kuwa mbunge huyo si mshukiwa wa kosa lolote hivyo hakuna sababu ya kutiwa kwake mbaroni ilivyodaiwa na wandani wa Rigathi mitandaoni.
Inspekta jenerali aidha amesema wameanzisha uchunguzi kuhusu matukio yaliyosababisha kushambuliwa kwa Gachagua na wandani wake.
Akizungumzia suala hilo, Kanja amewataka Wakenya wenye taarifa zinazoweza kusaidia kukamatwa kwa washukiwa waliovamia mazishi hayo kuripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu nao.
Akihutubia wanahabari katika makao makuu ya DCI hapo jana, Seneta wa Kiambu Karungo Wa Thang’wa alidai kuwa Mwathi alitekwa nyara na wanaume wasiojulikana waliokuwa kwenye gari nyeusi aina ya Subaru.
“Tumekuja hapa DCI kutaka uchunguzi wa haraka kuhusu kilichojiri leo. Hii ilikuwa jaribio la kumuua Rigathi Gachagua na lilitekelezwa na wahuni waliokodiwa na serikali,” Seneta huyo alisema.
“Pia tumekuja hapa kwa sababu tunataka kuambiwa aliko aliyekuwa mbunge Peter Mwathi ,” Thang’wa aliongeza.