Serikali ya Kenya kwa mara ya kwanza imezindua zoezi la kuhesabu wanyama pori kote nchini katika juhudi za kuwahifadhi wanyama hao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa sensa hiyo katika mbuga ya wanyama ya milima ya Shimba, waziri wa Utalii Najib Balala imesema sensa hiyo inalenga kupata jumla ya idadi ya wanyama pori na eneo walipo.

Zoezi hilo litajumuisha wanyama wanaoishi nyikani katika maeneo tofauti nchini na pia majini.

Amesema huenda baada ya zoezi hilo idadi ya baadhi ya wanyamapori waliohesabiwa hapo awali ikaongezeka kwani sio maeneo yote yalijumuishwa.

Serikali inalenga kutumia hesabu hiyo kubaini idadi ya wanyamapori katika maeneo tofauti nchini na kufahamu tishio kwa wanyama hao ili kuweka mikakati ya kuwalinda.