Kenya kwa mara ya kwanza imeandikisha idadi kubwa ya maafa yanayosababishwa na ugonjwa wa corona baada ya watu 24 kufariki katika muda wa saa Ishirini na nne zilizopita.

Hii inafikisha 1,154 idadi ya wagonjwa waliofariki kutokana na ugonjwa huo tangu kisa cha kwanza kiliporipotiwa nchini mnamo mwezi Machi mwaka huu.

Waziri wa afya Mutahi Kagwe katika taarifa amesema watu wengine 1,344 wamekutwa na ugonjwa huo baada ya kupima sampuli 7,162 na kufikisha idadi ya visa hivyo kuwa 64,588.

Nairobi imeandikisha visa 322, Kiambu 221, Mombasa 133, Laikipia 72, Uasin Gishu 66 na Kericho 65.

Watu waliopona katika muda huo ni 436 na hivyo kufikisha idadi hiyo kuwa 43,095.

Hadi kufikia sasa, waziri Kagwe amesema wahudumu wa afya wapatao 2,108 wameambukizwa virusi hivyo vya corona. 1,074 kati yao ni wanaume huku wanawake wakiwa 1,034. Wahudumu wa afya waliofariki kutokana na ugonjwa huo kufikia sasa ni 22.

Wagonjwa waliolazwa hospitalini ni 1,266, wanaoshughulikiwa nyumbani ni 5,898. 58 wamelazwa katika chumba cha watu mahututi ICU.