Muwaniaji huru kwenye uchaguzi mdogo wa Msambweni Sharlet Mariam amejiondoa kwenye kinyanganyiro hicho na badala yake kutangaza kumuunga mkono muwaniaji wa chama cha ODM Omar Boga.

Mariam aliyekuwa amejiuzulu kutoka chama hicho amesema amechukua uamuzi huo baada ya kukutana na kiongozi wa ODM Raila Odinga ambaye alimshawishi kumuunga mkono Boga ili wahakikishe kuwa kiti hicho kinasalia cha chama hicho.

Awali, muwaniaji huyo alijipata katikati ya mzozo wa chama cha Jubilee wakati naibu rais William Ruto alifika ghafla katika makao makuu ya chama hicho Pangani na kutaka atangazwe mgombea wa chama hicho katika uchaguzi huo.

Hata hivyo hilo halikufua dafu kwani chama cha Jubilee kilisema hakitakuwa na muwaniaji kwenye uchaguzi huo kwa sababu ya handisheki.

Waakazi wa Msambweni wataelekea debeni Disemba 15 kumchagua mrithi wa Suleiman Dori aliyefariki mnamo mwezi Machi mwaka huu.