Hakuna kazi ambayo nimepatiwa na rais Uhuru Kenyatta na nikakataa kufanya, amejitetea naibu rais William Ruto.

Akizungumza alipoendelea na misururu ya mikutano na viongozi katika afisi zake Karen, Nairobi, Ruto amesema amefanya kazi zote alizopewa na rais na kuwashutumu wanaodai kuwa hajawajibikia majukumu yake ipasavyo.

Amewataka wakosoaji wake wajibidiishe kufanya kazi zao na wala sio kumfuata fuata saa zote.

Wakosoaji wa Ruto akiwemo naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe waliibua maswali baada yake kukkosa kuhudhuria kongamano lililoandaliwa katika ukumbi wa mikutano KICC jijini Nairobi na kuongozwa na rais Uhuru Kenyatta kujadili hatua zilizopigwa katika kupambana na janga la corona.