Rais Uhuru Kenyatta hii leo anatazamiwa kulihutubia taifa kutoa mustakabali katika vita dhidi ya janga la corona.

Rais ameratibiwa kukutana na kamati ya dharura kuhusu COVID-19 kwa njia ya mtandao kabla ya kutoa hotuba kwa taifa.

Miongoni mwa masuala ambayo anatazamiwa kuyagusia ni ufunguzi wa shule na kafyu ambayo imekuwa ikitekelezwa kuanzia saa tatu usiku hadi saa kumi asubuhi.

Mwanaharakati wa kutetea haki za kijamii Fredrick Ogweno anasema wengi wa wakenya wanaumia kutokana na baadhi ya masharti hayo ikiwemo amri ya kutotoka nje ambayo imeathiri biashara kadha na anamtaka kuyalegeza.

Hata hivyo waatalamu wa afya wakionya dhidi ya ufunguzi kiholela kuwa huenda ukachangia maambukizi ya virusi hivyo nchini.

Hadi kufikia sasa, watu 38, 115 wameambukizwa virusi hivyo nchini, miongoni mwao, watu 24, 621 wakipona na wengine 691 wakifariki.