Idadi ya vifo kutokana na mafuriko imepanda hadi watu 289 baada ya watu wengine 12 kuaga dunia chini ya masaa 24 yaliyopita
Wizara ya usalama wa ndani katika taarifa yake ya kila siku kuhusu hali ya mafuriko imesema kuwa watu 188 wamepata majeraha kutokana na mafuriko huku wengine 75 wakiwa hawajulikani waliko.
Wizara hio aidha imedhibitsha kuwa idadi jumla ya familia zilizolazimishwa kuhama makwao imefika 57,120 watu walioathirika moja kwa moja ikiwa takriban watu 285,600.
Baadhi ya kaunti zilizoathirika zaidi kwa muda wa saa 24 zilizopita ni Tana River, Garissa, na Lamu .
Inakadiriwa kuwa ekari 168,092 ya mazao imeharibiwa huku mifugo 8,722 wakifa maji.
Serikali imehakikishia wakenya usalama wao huku ikiahidi kuendelea kutoa taarifa kwa wakati kuonya kuhusu maeneo yaliyo kwenye hatari ya kufurika.
Haya yanajiri huku hali ikitarajiwa kuboreka baada ya idara ya utabiri wa hali ya anga kudokeza kuwa viwango vya mvua vimepungua hali iliyochangia agizo la Rais William Ruto la shule kufunguliwa.