Baraza la magavana limetangaza kurejesha shughuli za kawaida katika serikali za kaunti siku moja baada ya maseneta kukubaliana kuhusu mfumo utakaotumika kugawa mapato.
Mwenyekiti wa baraza hilo Wycliffe Oparanya amewahongera rais Uhuru Kennyatta na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga kwa kuingilia kati na kutatua mgogoro uliokuwa unazingira mswada wa ugavi wa mapato.
Haya yanajiri huku waziri wa Fedha Ukur Yattani akisema kaunti zitapokea Sh60b kufikia Jumatatu wiki ijayo baada ya maseneta kuafikia makubaliano kuhusu mfumo utakaotumika kugawa pesa katika serikali za kaunti.
Yatani anasema pesa hizo ni kati ya Sh316b ambazo serikali za kaunti zilitengewa kwenye kipindi cha matumizi ya fedha mwaka 2020-2021.
Wakati uo huo
Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amepongeza juhudi zilizowekwa na rais Uhuru Kenyatta katika kutanzua utata uliokuwa unazingira mswada wa ugavi wa mapato.
Odinga katika taarifa amefafanua kuwa rais Kenyatta alisaidia kutatua mgogoro huo uliotatiza shughuli katika serikali za kaunti alipoahidi kutoa Sh50b kwa serikali za kaunti kipindi kijacho cha matumizi ya pesa za serikali.
Kinara huyo wa ODM vile vile amesifia hatua ya bunge la Senate kutumia ahadi hiyo ya rais kutanzua mgogoro huo uliosababisha magavana kusitisha shughuli muhimu katika serikali za kaunti.