HANDSHEKI YANUKIA WAFUASI WA ODM WAKIFURIKA KATIKATI MWA JIJI LA NAIROBI

0

Wafuasi wa Kinara wa Upinzani Raila Odinga wamefurika katikati mwa jiji la Nairobi Odinga akitarajiwa kutia saini makubaliano na Rais William Ruto leo hii.
Wafuasi hao wameleezea kushabikia muungano baina ya Odinga na Ruto wakisema utasaidia kuimarisha utangamano wa kitaifa.

“Sisi kama ODM lazima tuingie serikalini, mama mboga, mtu wa bodaboda, wajane sote lazima tuingie serikalini.” Mmoja wa wafuasi hao amesema.

Wafuasi hao ambao kwa sasa wako nje ya afisi za Gavana wa Nairobi iliyoko City hall wamekashifu wanaopinga muungano wa kisiasa kati ya Raila na Ruto.

Wamesema chama cha ODM kimeshiriki siasa za upinzani kwa muda mrefu na ni wakati wao kufaidi minofu ya serikali.

“ Kila baada ya uchaguzi kuna mgogoro, sasa viongozi wetu wameamua kuungana na kuna watu wanaopinga muungano, watu hao ni maadui wa nchi.” Mfuasi mwingine amedokeza.

Rais William Ruto kwa sasa anafanya mkutano wa Kundi la Wabunge (PG) na Wabunge washirika katika Ikulu ya Nairobi.

Odinga na Ruto wanatarajiwa kutia saini makubaliano katika jengo la KICC.

Muungano wao unatarajiwa kumpiga jeki Rais Ruto anapoonekana kuanza kampeni za kusaka hatamu ya pili uongozini.

Muungano huo aidha utakuwa pigo kwa upinzani ukiongozwa na Naibu wa Rais wa zamani Rigathi Gachagua ambao umekua ukichumbia Odinga kujiunga nao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here