Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua ameilaumu serikali ya Kenya Kwanza baada ya machafuko kuzuka katika hafla ya maombi iliyoandaliwa na mkewe Dorcas Rigathi siku ya Jumamosi.
Wakati wa hafla hiyo iliyoandaliwa mjini Nyeri, Maina Njenga, akiandamana na vijana, walivamia na kutatiza hafla hiyo.
Dorcas na Naibu Gavana wa Nyeri David Kinarire walilazimika kuondoka kwenye hafla hiyo baada ya kuhofia usalama wao.
” Kutumia kiongozi wa genge la uhalifu lililoharamishwa kuvuruga maombi ya amani na kuchafua madhabahu ndilo jambo la chini zaidi ambalo Serikali inaweza kufanya,” Gachagua amesema katika ukurasa wake kwenye mtandao wa X.
Mara tu baada ya Dorcas kuondoka, Njenga alienda kwenye hema alipokuwa ameketi na kuchukua nafasi yake.
Gachagua na Njenga wamekuwa wakizozana kwenye hafla za umma huku wadadisi wa masuala ya kisiasa wakidai kuwa Maina Njenga anatumiwa na serikali ili kupunguza umaarufu wa Gachagua katika eneo la Mlima Kenya.
Akizungumza katika hafla hiyo, Njenga alimshauri Gachagua kuacha siasa za ukabila na badala yake aendeleze umoja nchini.
“Tusiwe tunazungumzia siasa za Mlima Kenya kila wakati. Tuungane kama taifa kwa sababu Kenya ni yetu sote,” Njenga alishauri.