Wabunge wameidhinisha waziri wa usalama wa ndani Profesa Abraham Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais.
Wabunge 236 walipiga kura kumuidhinisha Kindiki katika vikao vilivyokamilika alasiri hii.
Hakuna mbunge aliyejiondoa kwenye kura hio au kupiga kura dhidi ya uteuzi wa Kindiki.
Haya yanajiri kufuatia kuteuliwa kwake na Rais William Ruto asubuhi ya leo.
“Uteuzi huo unatangazwa kupitishwa na Bunge na Spika atawasilisha matokeo kwa rais na spika pia atatia saini notisi ya gazeti rasmi la serikali kuhusu hili,” Spika Moses Wetangula alisema.
Hii sasa inamaanisha kuwa Rais Ruto atamteua Kindiki kama msaidizi wake mkuu kabla ya kuapishwa kwake na Msajili wa Mahakama.
Kindiki alikuwa amepigiwa upato kuwa mwaniaji mwenza wa Rais Ruto katika uchaguzi mkuu uliopita ila akakosa nafasi hio baada ya kiongozi wa Taifa kuteua Gachagua.
Hata hivyo amerejea kidedea baada ya ndoa ya Rais na Naibu wake kuingia doa kufuatia mivutano ya kisiasa.
Miongoni mwa waliokuwa wamependekezwa awali kuridhi Gachagua ni pamoja na Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata na Mwenzake wa Kirinyaga Anne Waiguru.