Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amelaani mauaji ya mwanaharakati na mwanasiasa kutoka Molo Richard Otieno ambaye aliuwawa kwa kukatwakatwa kwa shoka na watu wasiojulikana siku ya Jumamosi.
Kupitia akaunti yake kwenye mtandao wa X, Gachagua ametaka uchunguzi uharakishwe ili kuhakikisha wahusika wa mauaji hayo ya kinyama wanakamatwa na kujukumishwa kisheria.
Naibu rais huyo wa zamani aidha amekosoa serikali kwa ukimya wake kuhusu suala hilo akitaka hatua za haraka zichukuliwe.
“Serikali ya Kenya haiwezi kuendelea kukaa kimya kuhusu suala hili,”Gachagua amesema.
Otieno aliyewania pasi na mafanikio uwakilishi wadi wa Elburgon kwenye Uchaguzi mkuu uliopita alikuwa miongoni mwa wakosoaji wa serikali na mbunge wa Molo Kimani Kuria.
Gachagua ameomboleza kifo cha mwanaharakati huyo akitoa wito wa stahamala nchini akidai kuwa mauaji hayo yanadhihirisha jaribio la utawala wa sasa kuzima upinzani nchini.
Gachagua ambaye miezi za hivi karibuni amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ameonya kuwa ukandamizaji wa wapinzani wa Kenya Kwanza na uongozi wake unafika viwango vya kutisha.
“Mauaji ya kutisha na ya kikatili ya Richard Otieno wikendi ni shuhuda tosha ya mkakati mwingine wa kuzua hofu miongoni mwa wakenya katika mkakati wa kuwanyamazisha wakosoaji wa serikali,” Gachagua amesema.
“Inawezekanaje taifa kama Kenya kuteleza na kugeuka kuwa nchi ambapo watoto na wanawake hawana uhuru?” ameuliza Gachagua.
Wakazi wa Molo wenye ghadhabu hapo jana walichukua mwili wa mwanaharakati huyo kutoka makafani na kuupeleka hadi kituo cha polisi cha Elburgon.
Baada ya Hapo waliandamana wakiwa wamebeba mwili huo kuelekea nyumbani kwa mbunge wao Kuria Kimani wakimtaka kuwategulia kitendawili cha mauaji ya Otieno ambaye alikuwa mkosoaji wake mkuu.