Naibu Rais Rigathi Gachagua asubuhi ya leo amefanya mkutano na zaidi ya maseneta 10 kutoka eneo la Mlima Kenya.
Kulingana na Gachagua, mkutano huo umeangazia ukaguzi wa ufanisi wa mfumo wa ugatuzi wa serikali katika kaunti zao.
“Nilikuwa na Mkutano wenye fanaka na Maseneta kutoka Kaunti kumi na moja, kukagua mafanikio ya Ugatuzi katika kaunti zao,” Amesema Gachagua.
Naibu Rais amesisitiza kuwa Ushirikiano na viongozi ni njia nzuri ya kupata maoni ya wananchi kuhusu miradi inayotekelezwa na serikali kuu.
“Mazungumzo ya mara kwa mara na viongozi waliochaguliwa ni chachu ya maendeleo kwa watu wetu. Pia ni jukwaa bora la maoni juu ya kile waajiri wetu wanachofikiria na kuhisi kuhusu uongozi wetu.”
Maseneta hao ni pamoja na Kathuri Murungi (Meru), Joe Nyutu (Murang’a), Mwenda Gataya (Tharaka Nithi), Karungo Thang’wa (Kiambu), Alexander Mundigi (Embu), na Methu Muhia (Nyandarua).
Wengine ni Kamau Murango (Kirinyaga), Wahome Wamatinga (Nyeri), Tabitha Karanja (Nakuru), Joseph Kamau Githuku (Lamu), John Kinyua (Laikipia) na seneta mteule Veronica Maina.
Mkutano huo unajiri wakati ambapo Gachagua anakabiliwa na uhasama mkuu wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya.