FANYENI MTIHANI WA MWISHO WA MUHULA- WAZIRI MIGOS ARAI USIMAMIZI WA VYUO VIKUU

0

Waziri wa elimu Julius Migos amehimiza usimamizi wa vyuo vikuu vya umma nchini kuandaa mitihani ya mwisho wa muhula iwapo wameridhika kwamba wanafunzi wamepokea mafunzo ya kutosha.

Hii ni kufuatia mgomo wa wahadhiri ambao umeathiri masomo vyuoni kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Akizungumza baada ya usambazaji wa mitihani ya KCSE kaunti ya Nyamira, Migos amesema wizara yake inanuia kusaka suluhu la kudumu kwa tatizo la mgomo unaoendelea.

“Sio jambo la haki kwa mwanafunzi kutumia kipindi cha miaka tisa akisaka cheti cha shahada. Tunasaka suluhu kwa matatizo yanayokumba vyuo vyetu vikuu.” Amesema Migos.

Hayo yakijiri, Wahadhiri kutoka vyuo vikuu vya umma wamefanya maandamano kuanzia katika chuo kikuu cha Nairobi na kuelekea katika majengo ya bunge, pamoja na afisi za waziri wa elimu na hazina ya kitaifa.

Wakiongozwa na katibu mkuu wa muungano wa wahadhiri UASU Constantine Wasonga, wahadhiri wameapa kutorejea kazini hadi pale matakwa yao yanayojumuisha nyongeza ya mishahara na bima ya afya yatekelezwa.

“Makubaliano ilikuwa ni nyongeza ya asilimia 9, asilimia saba na asilimia nne kwa ngazi tofauti tofauti ya wahadhiri.”amesema Wasonga.

Mwenyekiti wa UASU Grace Nyongeza amesema ni sharti mwajiri wa wahadhiri kutekeleza kikamilifu mkataba wa makubaliano (CBA) ulioafikiwa kati yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here