Wauguzi wa hopsitali ya Mbagathi jijini Nairobi ambacho ni kituo muhimu cha kuwatenga na kuwatibu watu wanaoonesha dalili za kuwa na virusi vya Corona wamesusia kazi.
Wahudumu hao wa afya wamegoma kulalamikia kutopewa kwa vifaa watakavyojikinga navyo wanapowashughulikia wagonjwa na hivyo kuhatarisha maisha yao.
Wauguzi hao wanagoma wakati ambapo serikali ya Kenya inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuzuia kuenea kwa virusi hivyo ikiwemo kufunga shule na kupiga marufuku mikutano ya hadhara.
Wauguzi hao wanasema licha ya hospitali ya Mbagathi kuwa kituo muhimu katika kuwashughulikia watu walio na dalili za virusi vya Corona, serikali imekosa kuwapa vifaa hitajika kujikinga kwani kwa kuwashughulia wagonjwa hao, watakuwa wanahatarisha maisha yao kwa mujibu wa Boaz Onchari ambaye ni mwenyekiti wa Wauguzi kaunti ya Nairobi.
Anasema licha ya waziri wa afya Mutahi Kagwe kusema kuwa watapewa vifaa hivyo, hiyo imesalia kuwa ahadi wanayosubiri kutekelezwa kwake.
Wakati uo huo, shule zote zimefungwa kufuatia agizo la rais Uhuru Kenyatta siku ya Jumapili katika juhudi za kuzuia kusambaa kwa virusi hatari vya corona.
Waziri wa elimu Profesa George Magoha amezitaka shule kuhakikisha kuwa wanafunzi katika shule za mabweni wanapelekwa nyumbani na mabasi ya shule na iwapo ni sharti wakomboe magari ya uchukuzi wa umma, ni sharti mabasi hayo yasiwabebe raia wengine.
Nacho chuo kikuu cha Nairobi kikiongozwa na naibu Chansela Stephen Kiama imesitisha shughuli za masomo kuambatana na agizo la rais.
Hadi kufikia sasa Kenya imeripoti visa vitatu vya Corona huku mataifa mengine yakiendelea kuweka mikakati kupambana navyo ikiwemo kufunga mipaka, kupiga marufuku mikutano ya hadhara na kuhimiza usafiri wa hali ya juu.