Tume ya kutetea haki za kibinadamu nchini Kenya (KHRC) inamtaka rais Uhuru Kenyatta kutumia mamlaka yake ya kikatiba na kutangaza hali ya hatari nchini humo kutokana na janga la kimataifa la virusi vya corona.
KHRC katika taarifa inasema kutangaza hali ya hatari sawa na iliyofanya Marekani, Uhispania pamoja na mataifa mengine itafanikisha vilivyo vita dhidi ya virusi hivyo na kupunguza kutangamana kwa watu na hivo kudhibiti kuenea kwake.
Mkurugenzi mkuu mtendaji wa shirika hilo kongwe la kutetea haki za kibinadamu KHRC Davis Malombe anasema ilivyo kwa sasa, serikali imetangaza hatua mbalimbali kukabiliana na coronavirus ila shughuli za kawaida zinaendelea jambo linalohatarisha maisha ya Wakenya haswaa wanapotangamana.
Anaeleza kuwa iwapo rais atatumia mamlaka yake kikatiba na kutangaza hali ya hatari, basi atakuwa amewajibikia vilivyo jukumu lake kikatiba kwani kimsingi anaruhusiwa kufanya hivyo wakati kama huu.
Hayo yakjiri,
Hospitali kuu ya kitaifa ya Kenyatta (KNH) imetangaza kudhibiti idadi ya watu wanaoruhusiwa kuingia katika hospitali hiyo kuwaona wagonjwa wao waliolazwa katika harakati za kuuzuia kuenea kwa virusi vya corona.
Afisa mkuu mtendaji wa hospitali hiyo Evanson Kamuri anasema watakaoruhusiwa kuwaona wagonjwa sharti wazingatie usafi wa hali ya juu na pia kuvalia magwanda ya kuwakinga na maambukizi.