Adamson Bungei ameondolewa kutoka kwa wadhfa wake wa kamanda wa Polisi jijini Nairobi katika mageuzi ya hivi punde kwenye uongozi wa polisi humu nchini.
Katika mageuzi hayo Bungei amerejeshwa katika makao makuu ya polisi na kutajwa kama mkurugenzi wa operesheni katika idara ya polisi naye kamanda wa polisi eneo la Pwani George Sedah akiteuliwa kuchukua nafasi ya Bungei jijini Nairobi.
Kamanda wa Polisi kaunti ya Kiambu Michael Nyaga ameteuliwa kama msemaji wa Polisi akichukua nafasi ya Resillah Ouma ambaye ameteuliwa kama kamanda wa Kitengo cha Ulinzi wa Kidiplomasia.
Kamanda wa polisi kaunti ya Kwale Ali Nuno Amepandishwa cheo na kutajwa kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani kuchukua nafasi ya Sedah.
Mkuu wa Maabara ya Kitaifa ya Uchunguzi katika makao makuu ya DCI Dkt Mwangi Wanderi amehamishwa hadi Vigilance House na kuteuliwa mkurugenzi wa rasilimali nguvu kazi akibadilishana wadhfa na Rosemary Kuraru ambaye sasa ataongoza maabara ya Uchunguzi.
Mkuu wa Kitengo cha Uhalifu katika DCI Michael Sang’ amehamishwa hadi eneo la Mashariki kama mkuu wa DCI eneo hilo.
Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja ametaja mabadiliko hayo kuwa ya kawaida ili kuimarisha utendakazi katika huduma.