Kisa cha kutekwa nyara kwa mwakilishi wadi wa Kaunti ya Wajir Yussuf Hussein Ahmed kimechukua mkondo mwingine, Bob Njagi mmoja wa watu waliotekwa nyara eneo la Kitengela akifichua kuwa alikuwa kizuizini na mwakilishi wadi huyo.
Kwenye mahojiano usiku wa kuamkia Leo, Njagi amefichua kuwa mwakilishi wadi huyo aliletwa nyakati za usiku na kufungwa kwenye chumba mkabala na chake.
“Tunaweza kucheka kuhusu suala hili wakati mwingine lakini nataka kusema hapa kwamba MCA wa Kaunti ya Wajir alikuwa chumba karibu na nilipokuwa … nilipata fursa ya kuchungulia kwenye tundu la funguo na nikamwona,” Njagi alisema.
Njagi amesema kuwa Hussein aliletwa usiku wa kuamkia Ijumaa, Septemba 13, 2024, na kufungiwa karibu na chumba chake.
Kwa mujibu wa Njagi, Mwakilishi wadi huyo aliletwa wakati wa usiku tukio ambalo halikuwa kawaida jambo lililomfanya kupeleleza kufahamu taarifa kuhusu mfungwa huyo mpya.
“Kupitia uchunguzi wangu mwenyewe, niligundua kwamba alikuwa na asili ya Kisomali na mara baada ya kuachiliwa, nilifanya upekuzi wangu mwenyewe na kugundua kuwa siku hiyo hiyo, Ijumaa, Septemba 13, kulikuwa na mtu ambaye alitekwa nyara katika Barabara ya Enterprise na ndiye yule yule aliyefikishwa tulipo.”
Njagi hata hivyo amedokeza kuwa alipoondoka kizuizini aliwacha mwakilishi wadi huyo akiwa bado yu hai.
Madai ya mwanaharakati huyo yanajiri huku Mahakama Kuu ikiagiza Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja kufichua aliko mwakilishi wadi huyo Yussuf Hussein Ahmed ndani ya siku 14.
Mwezi mmoja baada ya kutoweka, mwili uliopolewa katika Ziwa Yahud ambao uliaminika kuwa MCA aliyetoweka; hata hivyo uchunguzi wa DNA ulibainisha kuwa sio wake.