Spika wa bunge la kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi amejiuzulu kutoka kwa wadhfa wake baada ya miezi kadhaa ya malumbano ya uongozi katika jumba la City Hall.
Katika kikao na wanahabari afisini mwake mapema hii leo, Elachi amesema vurugu za kila mara katika bunge hilo zimemfanya kujiuzulu na kusema naibu wake John Kamangu atakuwa kaimu spika.
Haya yanajiri siku chache baada ya Waziri wa Usalama wa ndani Fred Matiangi kueleezea kusikitishwa kwake na vurugu za mara kwa mara City Hall na kusema atashauriana na asasi husika kupata suluhu la kudumu.
Elachi amewataka waakilishi wadi wa jiji la Nairobi kuunga mkono mkurugenzi wa shirika la NMS Mohammed Badi na kumtaka Gavana Mike Sonko kukomesha malumbano ya kila mara.
Amesema anamshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kumpa nafasi ya kuliongoza bunge hilo na pia kumshukuru kinara wa ODM Raila Odinga kwa ushauri wake.
Elachi amedokeza kuwa atakuwa anaandika kitabu “Chronicles of City Hall” kuelezea masaibu yaliyomkumba katika muda ambao amehudumu.
Elachi alichaguliwa tarehe sita Septemba mwaka 2017 kuwa spika wa jiji, lakini uongozi wake umekumbwa na migogoro baada ya kutofautiana na Gavana Mike Sonko na baadhi ya waakilishi wadi.
Oktoba mwaka uliopita, 2019, mahakama ilimrejesha Elachi afisini baada ya kutimuliwa na waakilishi wadi kwa madai ya uongozi usiofaa.
Septemba mwaka 2018, waakilishi wadi 103 kati ya 107 walipiga kura kuunga mkono hoja ya kumtimua spika huyo.
Bunge hilo la kaunti kwa sasa liko likizoni na linatazamiwa kurejelea vikao vyake mwezi wa tisa mwaka huu ambapo kibarua chao cha kwanza kitakuwa kumtafuta spika mwingine.