Takriban watu 14 Wameaga dunia asubuhi hii trela ilipogongana na matatu katika eneo la Migaa, Molo, kwenye Barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.
Maafisa wa Polisi wamesema watu wote 12 waliokuwa kwenye matatu ya Kitale Shuttle na 2 waliokua kwenye trela hio walifariki papo hapo katika kisa hicho kilichotokea mwendo wa saa tisa asubuhi.
Kwa mujibu wa msemaji wa Polisi Michael Muchiri, waathiriwa hao ni pamoja na wanaume tisa, wanawake wanne na mtoto mmoja.
Muchiri ametahadharisha wanaotumia barabara ya Nakuru- Eldoret kuwa waangalifu kutokana na wingi wa ajali katika barabra hiyo.
” Migaa ni miongoni mwa maeneo hatari katika barabara ya Nakuru- Eldoret, na tunawahimiza madereva wa magari kuwa waangalifu wanapokaribia huko,” amesema Muchiri.
Mwezi Agosti Mwaka jana Takriban watu 14 walifariki na wengine kadhaa kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi inayomilikiwa na kampuni ya Coast Bus katika eneo hilo la Migaa.
Muchiri amesema uchunguzi wa awali umebainisha kuwa dereva wa trela alishindwa kuimudu kabla ya kugonga matatu.
Zaidi ya watu 4000 huuawa kila mwaka katika ajali nchini huku Maelfu ya wengine wakisalia na majeraha ambayo yanaadhiri uwezo wao wa kuendesha shughuli zao za kila siku.
Takwimu zilizotolewa na polisi zinaonyesha kuwa takriban watu 4,282 waliuawa katika ajali kati ya Januari na Novemba 2024 ikilinganishwa na 3,901 katika kipindi kama hicho mwaka wa 2023.
Muchiri amedokeza kuwa polisi wana mpango wa kuanzisha kampeni ya kukabiliana na ongezeko la ajali barabarani.