BABA YAO AHUKUMIWA MIAKA 12 JELA.

0

Gavana wa zamani wa kaunti ya Kiambu Ferdinand Waititu amehukumiwa kifungo cha miaka kumi na miwili gerezani au alipe faini ya shilingi milioni 53.

Hii ni baada ya mahakama kumpata na hatia katika sakata ya ufisadi ya shilingi milioni 588 iliyohusisha utoaji zabuni ya kukarabati barabara bila kufuata utaratibu ufaao wakati akiwa gavana.

Mkewe Susan Wangari ambaye walishtakiwa pamoja katika kesi hiyo amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja au faini ya shilingi laki tano.

Wengine ambao wamepatikana na hatia kwenye sakata hiyo ni pamoja na mkurugenzi wa kampuni ya Testimony enterprise Charles Chege ambaye amehukumiwa kifungo Cha miaka tisa au kulipa faini ya shilingi milioni 295 pamoja na baadhi ya maafisa wa kaunti hiyo wakati wa uongozi wa Waititu.

Katika uamuzi wake kwenye kesi hiyo hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani Thomas Nzioki amempata Waititu na makosa yakiwamo ufisadi, mgongano wa kimaslahi, utakatishaji wa fedha na matumizi mabaya ya ofisi aliyokua akihudumu.

“Hitimisho lisiloweza kuepukika ni kwamba Waititu atawajibika kwa mgongano wa maslahi kwa kujipatia faida ya shilingi milioni 25 isiyo ya moja kwa moja kutoka kwa kampuni ya Testimony,” alisema hakimu Nzioki katika hukumu yake.

Hakimu Nzioki alibaini kuwa Waititu alifeli kuheshimu katiba kwa kushindwa kulinda mali ya umma.

“Upande wa mashtaka uliweza kudhibitisha kuwa Waititu alishindwa kuzingatia maadili ya utawala wa kitaifa wala kulinda fedha za umma alipopokea shilingi milioni 25 kutoka kwa kampuni ya Testimony baada ya kutoa zabuni tata.” aliongeza hakimu.

Kufuatia hukumu hiyo wahusika wamepigwa marufuku kuhudumu katika nafasi yoyote ile kwenye ofisi ya umma ndani ya kipindi cha miaka kumi ijayo.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here