Asilimia 70% ya wazazi wanaopata kipato cha chini katika maeneo mbalimbali jijini Nairobi wanahofia kuwa watoto wao watapata virusi vya corona kufuatia ufunguzi wa shule, umebaini utafiti uliofanywa hivi karibuni na kampuni ya utafiti ya TIFA.
Utafiti huo uliofanywa katika mitaa ya Kibra, Huruma, Mathare, Korogocho, Kawangware na Mukuru kwa Njenga umeonesha kuwa asilimia 73% ya wanawake wanahofu zaidi ikilinganishwa na asilimia 67% ya wanaume.
Hata hivyo asilimia 23% ya waliohojiwa wamesema hawana wasiwasi huku asilimia 7% wakisema hawana uhakika.
Utafiti huu uliofanywa kati ya Septemba 24 na Octoba 2 mwaka huu umeonyesha kuwa wazazi hao wanahofia kuwa masharti ya wizara ya afya hayatekelezwi ipasavyo kutokana na changamoto zilizoko katika shule mbalimbali ikiwemo ukosefu wa nafasi, maji safi miongoni mwa zingine.
Haya yanajiri siku moja baada ya shule kufunguliwa huku wanafunzi wa darasa la nne, darasa la nane na kidato cha nne wakiripoti shuleni licha ya changamoto mbalimbali.