ALIYEKUWA MPENZI WA MWANARIADHA REBECCA CHEPTEGEI DICKSON NDIEMA AMEFARIKI DUNIA

0
Rebecca Cheptegei.
Rebecca Cheptegei.

Aliyekuwa mpenzi wa mwanariadha Rebeca Cheptegei – Dickson Ndiema ameaga dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Moi jijini Eldoret.

Hospitali hio imethibitisha kuwa Ndiema alifariki usiku wa kuamkia leo katika chumba cha wagonjwa mahututi ICU alikokuwa amelazwa.

Ndiema alimvamia Cheptegei nyumbani kwake Trans Nzoia ambapo alimmwagia petroli na kumwasha moto tukio lilomsababishia majeraha ya asilimia 80 ya moto huku Ndiema akiungua kwa asilimia 30.

Babake Rebecca, Joseph Cheptegei, alilaumu maafisa wa polisi kwa kutochukua hatua za mapema baada ya bintiye aliyeshiriki kwenye mbio za marathon katika Olimpiki mwaka huu kupiga ripoti ya kutishiwa na Dickson.

“Mnamo Februari, walikuwa na mzozo na kijana huyu alitaka kumlaghai binti yangu na ikabidi atoroke. Tuliripoti suala hilo kwa polisi,” babake mwanariadha huyo aliambia kituo kimoja cha habari humu nchini.

Mwanariadha huyo ameratibiwa kuzikwa kwa taratibu za kijeshi siku ya Jumamosi nchini Uganda kwani alikuwa afisa wa Jeshi la Taifa Hilo (UPDF).

Uchunguzi wa maiti unatarajiwa kufanywa kesho katika hospitali ya MTRH kabla ya mwili kukabidhiwa kwa familia na jeshi la UPDF.

Ratiba ya mazishi inaonyesha kuwa marehemu atapelekwa nyumbani kwake Endebes kaunti ya Trans Nzioa siku ya Alhamisi ambapo wenyeji watapewa nafasi ya kumuaga kabla ya kusafirishwa hadi Bukwo nchini Uganda atakapozikwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here