Gavana Okoth Obado amepata afueni ya muda baada bunge la kaunti ya Migori kuhairisha vikao vya kujadili hoja ya kutokuwa na imani naye.
Spika wa bunge hilo Boaz Okoth amesema amechukua hatua ya kuhairisha vikao hivyo kwa sababu idadi kubwa ya waakilishi wadi waliofika kwa vikao vya leo ilifanya vigumu kwao kuzingatia masharti ya kuzuia msambao wa corona.
Okoth anasema ilikuwa vigumu kwao kukaa umbali wa mita moja unusu na hivyo akahairisha vikao hivyo hadi kesho asubuhi.
Haijabainika wazi iwapo hoja hiyo itakuwa miongoni mwa masuala ambayo watajadili kwani hadi kufikia sasa haijawasilishwa rasmi kwenye bunge hilo.
Waakilishi wadi walipigania kuingia kwenye vikao vya leo kwa hofu kuwa baadhi yao wangefungiwa nje wasipate nafasi ya kufanya uamuzi wa kumbandua afisini Obado anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi.
Chama cha ODM kinasisitiza kuwa Obado lazima angatuke madarakani kwani hawaungi mkono wanachama wao kuhusishwa na kashfa za ufisadi.