Kampuni ya usafiri wa umma Super Metro imepata afueni baada ya mahakama kuondoa kwa muda agizo la Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Usalama (NTSA) kufutilia mbali leseni yake ya kuhudumu.
Bodi ya Rufaa ya Leseni za Usafiri katika agizo lililotolewa Jumatatu asubuhi imeruhusu magari ya Super Metro kurejelea shughuli za uchukuzi wa umma mara moja lakini waendelee kuzingatia sheria.
Bodi hiyo ikiongozwa na wakili Adrian Kamotho imesema Super Metro haikupewa nafasi na NTSA kujitetea dhidi ya madai ya kutofuata sheria kadhaa zinazodhibiti sekta ya usafiri wa umma kabla ya leseni yao kufutiliwa mbali.
“Amri ya muda inatolewa kusitisha utekelezaji wa uamuzi wa Machi 18, 2025, kusimamisha shughuli za Super Metro Sacco Limited,” Kamotho aliagiza.
“Super Metro ina uhuru wa kuendelea na shughuli mara moja,” agizo la bodi hiyo limesema.
Bodi hiyo pia imeagiza rufaa iliyowasilishwa na Super Metro kusikilizwa kuanzia Alhamisi tarehe 27th Machi mwaka huu.
NTSA ilifutilia mbali leseni ya kuhudumu ya Super Metro kufuatia ukiukaji mbalimbali wa sheria za uchukuzi ikiwa ni pamoja na vyeti vya ukaguzi vilivyokwisha muda wake na ukosefu wa rekodi za vifaa vya kudhibiti mwendo.
Hatua ya NTSA ilijiri baada ya abiria kudaiwa kurushwa nje ya Super Metro na kuaga dunia baada ya mzozo na kondakta kuhusu nauli ya Shilingi 30 katika barabara kuu ya Thika.