Mahakama Kuu imesitisha utekelezwaji wa uamuzi wa bunge la Seneti la kumuondoa Rigathi Gachagua kutoka kwa wadhifa wa Naibu wa Rais.
Jaji Chacha Mwita aidha amesitisha mchakato wowote wa kuteua naibu wa Rais Mpya hadi Oktoba 24 mwaka huu.
“Wakati huo huo, agizo la muda limetolewa kusimamisha azimio la kudumisha mashtaka dhidi ya Naibu Rais,” alisema Jaji Mwita.
Jaji huyo aidha ameidhinisha ombi lililowasilishwa na Wakili Paul Muite kuwa kesi hiyo itangazwe kuwa ya dharura na faili hiyo kukabidhiwa kwa Jaji Mkuu Martha Koome.
Koome sasa atateua jopo litakalosikiliza na kuamua masuala ya kikatiba yaliyoibuliwa na upande wa Gachagua.
Ombi lingine limewasilishwa katika Mahakama Kuu jijini Nairobi likitaka Bunge la Kitaifa lizuiwe kujadili uteuzi wa Waziri Kithure Kindiki kuchukua nafasi ya Gachagua kama Naibu Rais.
Shirika la Sheria Mtaani Na wakili Shadrack Wambui wametaka maagizo ya kusitisha utekelezwaji wa Notisi kwenye gazeti rasmi la serikali iliyochapishwa na Spika wa bunge la Seneti Amason Kingi iliyotangaza wazi nafasi ya Naibu Rais.
Maseneta jana usiku walipiga kura kuunga mkono mashtaka matano kati ya 11 yaliyowasilishwa dhidi ya Gachagua katika hoja ya kumtimua iliyokuwa ikifadhiliwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.