GAVANA WA UASIN GISHU AFANYIA MABADILIKO BARAZA LA MAWAZIRI, AWATUMA MAAFISA 9 WAKUU KWA LIKIZO YA LAZIMA

0

Gavana wa Uasin Gishu Jonathan Bii amefanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri na kuwatuma kwa likizo ya lazima maafisa tisa wakuu wa kaunti hiyo.

Bii amesema hatua ya kuwatuma kwa likizo ya mwezi mmoja maafisa hao ni kuruhusu ukaguzi wa utendakazi wao na haja ya kufanya tathmini ya kina ya wafanyikazi ili kuimarisha utoaji wa huduma bora.

Katika mabadiliko hayo, Elijah Kosgey sasa atakuwa waziri wa elimu baada ya kuondolewa katika utumishi wa umma huku Dkt Sam Kotut akihamishwa kutoka kwa mazingira hadi Kilimo.

Edward Sawe amehamishwa kutoka kwa kilimo hadi ardhi huku Anthony Sitienei akihamishiwa maji kutoka kwa elimu , Johnstonne Kotut ameteuliwa kuwa mshauri wa masuala ya uchumi na Dkt Pius Kiplimo kuwa Mkuu wa wafanyikazi.

Bii alifanya mabadiliko hayo punde tu baada ya hafla iliyofanyika katika makao makuu ya kaunti hiyo ambapo aliwataka wakazi kupuuza propaganda zinazoongezeka za kisiasa katika eneo hilo.

“Puuza mambo yote hayo unayosikia na mwaka huu tuzingatie kazi na kazi,” amesema Bii.

Wakati huo huo, Naibu Gavana Evans Kapkea amesema wakati wa siasa utafika akimpongeza Gavana Bii kwa kupuuza kile alichokitaja kuwa “siasa duni”.

“Wakati wa siasa ukifika kila mtu atapata nafasi ya kueleza alichokifanya. Ikifika mwaka wa 2027 wakaazi wa Uasin Gishu wataamua,” Kapkea amesema.

Amesema wakazi wanapaswa kumuunga mkono gavana wao ili kutimiza ajenda yake ya maendeleo yenye vipengele kumi.

Bii amekuwa akikabiliwa na shinikizo kutoka kwa wakazi kuwatimua maafisa wa kaunti wasiochapa kazi ila kufikia sasa hakuna aliyetumwa nyumbani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here