RAIS RUTO ATOA MWONGOZO HATMA YA WAFANYIKAZI WA MASHIRIKA YATAKAYOVUNJWA

0

Rais William Ruto ametoa hakikisho kuwa hakuna atakayepoteza kazi, hata serikali inapoanza kuunganisha na kuvunja mashirika yake ambayo yana majukumu yanayooana.

Rais amesema kuwa watumishi wote katika taasisi zilizoathirika watahamishwa hadi mashirika mengine ya serikali.

Katika taarifa Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed, amesema uamuzi huo unalenga tu kurahisisha upatikanaji wa huduma za serikali na kupunguza matumizi yasiyofaa ya rasilimali za umma.

“Hakuna kazi zitakazopotea kwani wafanyikazi wote walioathiriwa wataingizwa katika Utumishi wa Umma,” imesema taarifa hiyo kwenye mtandao wa X.

“Hii inaambatana na dhamira ya kurahisisha shughuli za serikali na kukabiliana na ubadhirifu. Marekebisho hayo yatashughulikia upungufu wa kiutendaji na kifedha, kuboresha utoaji wa huduma na kupunguza utegemezi wa Hazina.”

Ufafanuzi huo unajiri kufuatia hofu kwamba maelfu ya watumishi wa umma wataachwa bila kazi baada ya Baraza la Mawaziri kuidhinisha uunganishaji, uvunjaji na uuzaji wa baadhi ya mashirika ya serikali.
Januari tarehe 21, Baraza la Mawaziri liliidhinisha kuunganishwa kwa mashirika 42 na mashirika 20 ili kupunguza gharama na kuongeza ufanisi.

“Mageuzi haya yametokana na kuongezeka kwa shinikizo la kifedha linalotokana na rasilimali haba za serikali, mahitaji ya huduma za umma za hali ya juu, na kuongezeka kwa mzigo wa deni la umma.” Amesema Hussein.

“Mashirika mengi ya serikali yametatizika kutimiza majukumu yao ya kimkataba na kisheria, na kusababisha mkusanyiko wa bili ambazo hazijakamilika za Sh94.4 bilioni kufikia Machi 31, 2024.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here