Kanisa Katoliki limejitokeza kukanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Kadinali mstaafu John Njue ameiaga dunia.
Katika Taarifa Kasisi Wallace Ng’ang’a Gachihi amesema kuwa Njue yu hai, na imewataka Wakenya kupuuza kile ambacho ametaja kama “uvumi ambao hauna msingi wowote”.
Kasisi Wallace amesema kuwa taarifa yoyote kuhusiana na afya ya Kadinali huyo mstaafu itatolewa kupitia vyanzo rasmi na vilivodhibitishwa vya kanisa la katoliki.
“Tunawaomba wote wajiepushe na taarifa ambazo hazijathibitishwa, hasa kuhusu masuala nyeti kama haya. Iwapo kutakuwa na mawasiliano rasmi kuhusu afya ya Kadinali au jambo lingine lolote, yatawasilishwa kupitia njia rasmi za Kanisa,” imesema taarifa hiyo.
Kasisi huyo aidha amerai wakenya kuendelea kumuombea Askofu Njue mwenye umri wa miaka 80.
“Tunaomba uendelee kumweka Kadinali Njue katika sala zako na tunamtakia afya njema na baraka tele.”
Hapo awali, taarifa zilizagaa mitandaoni kuwa Kadinali huyo alikuwa ameaga dunia, huku mada hiyo ikivuma kwenye orodha ya mijadala kuu katika mtandao wa X (Twitter).