Tume ya Utumishi wa Umma PSC imeorodhesha majina ya watu sita watakaopigwa msasa kujaza nafasi ya mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Kuu ya Kenya (CBK )
Sita hao ni pamoja na Abdikadir Aden, John Konchellah, James Wahome, Thomas Mwadeghu, Andrew Musangi na James Lopoyetum.
Tume hiyo imeratibu kuwapiga msasa, sita hao tarehe 12 Julai, huku wakenya wakitakiwa kuwasilisha taarifa yoyote inahusiana na waliorodheshwa kabla ya Julai 10.
“Wagombea wanapaswa kuwa kwenye ukumbi angalau dakika 15 kabla ya muda wa msasa kuanza, Wakenya walio na taarifa inayohusiana na wagombea waliochaguliwa kuwasilisha taarifa hizo mtandaoni kupitia anwani ya hodrands@publicservice.go.ke, “PSC ilisema.
Mgombea atakaeteuteuliwa atamrithi Mohamed Nyaoga aliyekamilisha mihula yake miwili ya miaka nane
Nyaoga aliteuliwa kwa mara ya kwanza katika wadhifa huo na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta mnamo Juni 2015 na kuchaguliwa tena kwa muhula wa mwisho wa miaka minne mwezi Juni 2019
Kulingana na Sheria ya CBK mwenyekiti wa bodi hiyo anaruhusiwa kuwa madarakani kwa kipindi cha miaka minne na kuruhusiwa tena kuendelea kwa muhula miaka minne zaidi baada ya kuteuliwa tena
Kwa mujibu wa Ibara ya 231 ya Katiba na kifungu cha 10-15 cha Sheria ya CBK, mtu anastahili kuwa mwenyekiti ikiwa ana shahada ya uzamili katika uchumi, fedha au sheria.
” Wagombea lazima wawe na uzoefu wa miaka 10 katika ngazi za juu za usimamizi katika uchumi, fedha au sheria, amabpo mwenyekiti ataitisha na kuongoza mikutano ya bodi ya CBK, sheria hiyo inasema”
Mwenyekiti anatathmini utendaji wa Gavana wa CBK, huamua sera ya benki (isipokuwa uundaji wa sera ya fedha) na kukagua jinsi taasisi inavyotumia rasilimali zake.