Rais William Ruto amesema watu milioni 7 waliochelewa kulipa mikopo yao ya Fuliza wameondolewa kutoka kwa orodha ya ofisi ya kumbukumbu ya mikopo na orodha nyingine za wenye kasoro ya kutolipa mikopo.
Rais Ruto alisema hatua hiyo itawapa Wakenya walioorodheshwa fursa mpya ya kupata huduma za mikopo kama vile Hazina ya Hasla.
Akizungumza katika Kanisa Katoliki la St Mary’s mjini Molo, Kaunti ya Nakuru, Rais alisema utawala wake una nia ya kutekeleza ahadi za kabla ya uchaguzi katika manifesto yake ya 2022.
Wakati wa kampeni zake kabla ya uchaguzi wa Agosti, Rais Ruto aliahidi kukagua orodha ya mikopo ili kufungua fursa ya kupata mikopo kwa watu waliozuiwa kukopa kutokana na orodha hiyo iliyo na sifa mbaya.
Kiongozi wa Nchi aliwasifu wenyeji wa Kaunti ya Nakuru ambao kufikia sasa wamekopa Shilingi bilioni 1.8 kutoka kwa Hazina ya Hasla huku kiwango cha ulipaji wa mikopo hiyo kikiwa cha asilimia 73.
“Inapendeza kwamba wakazi wa Kaunti ya Nakuru kufikia sasa wamekopa Shilingi bilioni 1.8. Kiwango chao cha malipo ni cha juu zaidi kwa asilimia 73,” Rais Ruto alisema.
Wakati huo huo, Rais aliwahakikishia Wakenya kwamba Serikali inachukua hatua kukabiliana na gharama ya juu ya maisha.
Alisema kupunguzwa kwa gharama za uzalishaji kutazaa matunda hivi karibuni katika kukabiliana na gharama kubwa ya maisha.
“Hatua tulizochukua ikiwa ni pamoja na kupunguza bei ya mbolea itazaa matunda hivi karibuni kwani wakulima watazalisha chakula kingi cha matumizi na cha ziada cha kuuza, hivyo basi kupunguza gharama ya maisha,” akasema Rais Ruto.
Alisema Kaunti ya Nakuru inakadiriwa kuzalisha kati ya magunia milioni 500 hadi 600 ya mahindi katika msimu ujao wa kuvuna.
Rais alimwagiza Waziri wa Ardhi Zachary Njeru, ambaye alikuwepo, kuchunguza njia za kutatua tahadhari zilizowekwa dhidi ya ardhi katika kaunti hiyo zinazozuia matumizi ya ardhi hizo.
Alisema Serikali itafanya kila iwezalo kutatua tatizo la tahadhari hizo katika eneo hilo ili kuhakikisha utoaji wa hati miliki kwa ufanisi.
Aidha Kiongozi wa Nchi alisema Serikali itatumia Shilingi milioni 100 kufadhili uanzishwaji wa vifaa vya kisasa vya kuhifadhia viazi katika kaunti hiyo.
Alibainisha kuwa Serikali itafadhili ujenzi wa viwanda
vitatu vya kuhifadhi viazi kwa njia ya barafu huko Molo na maeneo mengine mawili katika kaunti hiyo.
Rais Ruto alitangaza kuwa kazi ya ujenzi wa bwawa la Itare lililokwama itaanza hivi karibuni.
Naibu wa Rais Rigathi Gachagua aliwataka viongozi kushirikiana katika kutatua changamoto zinazowakumba Wakenya.
“Ni wakati wa viongozi kuweka kando masuala ya Uchaguzi Mkuu uliopita na kuangazia kuwatumikia wananchi,” akasema Bw Gachagua.
Gavana Susan Kihika alisema ujenzi wa vifaa vya kuhifadhia baridi utashughulikia changamoto zinazowakabili wakulima wa viazi katika eneo hilo.
Mbunge wa Mwala Vincent Musyoka aliwataka Wakenya kumruhusu Rais Ruto kutekeleza mipango inayolenga kuboresha uchumi wa nchi.
“Sote tunajua kuwa Rais Ruto alirithi matatizo yanayotukabili. Rais wetu ana mipango ya kubadilisha nchi hii. Hebu tumpe muda,” alisema Musyoka.
Viongozi waliokuwepo ni wabunge Kimani Kuria (Molo), Charity Chepkwony (Njoro), John Methu (Nyandarua), David Gikaria (Nakuru Town East), Joseph Tunoi (Kuresoi Kusini), Liza Chelule (Nakuru), George Gachagua (Ndaragwa), Jane Njeri ((Kirinyaga) na Benjamin Gathiru (Embakasi ya Kati).