Afrika lazima itengeneze miundombinu yake ili kuchochea biashara katika kanda.
Rais William Ruto alisema bara la Afrika lazima lianzishe ufadhili endelevu ili kuharakisha ukarabati wa miundomsingi yake.
Alisema serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo lazima washirikiane ili kuendeleza jambo hili.
Alibainisha kuwa ukosefu wa mfumo bora wa usafiri unaendelea kuzorotesha uwekezaji.
“Hii imefanya kuwa na gharama kubwa kufanya biashara, na hivyo kupunguza ushindani wa bara la Afrika,” alisema.
Rais pia alitoa wito wa kuharakishwa kwa kuanzishwa kwa mfumo wa pamoja wa malipo na suluhu ili kusaidia biashara kati ya nchi za Afrika.
“Mfumo huo utaundwa ili kuondoa changamoto za malipo ya mipakani; hii itaongeza kasi ya biashara ya ndani ya Afrika,” alisema.
Alisema hayo siku ya Jumatatu wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Eneo Huru la Biashara katika Bara la Afrika (AfCFTA) na Majadiliano ya Sekta ya Kibinafsi ya Afrika kuhusu AfCFTA jijini Nairobi.
Rais alitoa wito kwa nchi ambazo bado hazijatia saini na kuridhia AfCFTA kuungana na wenzao katika kuunda mfumo madhubuti wa kiuchumi duniani.
Alisema AfCFTA itachochea biashara ndani ya Afrika, kubuni nafasi za ajira, kuimarisha viwanda na kukuza ukuaji wa uchumi.
Ikiwa itatekelezwa ifikapo mwaka wa 2035, AfCFTA itasaidia kuwaondoa zaidi ya watu milioni 30 kutoka kwa umaskini uliokithiri.
Pia itapanua mauzo ya nje ya nchi za Afrika kwa takriban asilimia 80.
Rais alitoa wito kwa viongozi wa Afrika kuimarisha Umoja wa Afrika kwa kuiruhusu kufanya mazungumzo kwa niaba ya bara hilo.
“Tunaweza kujadiliana vyema ikiwa tuko pamoja.”
Rais wa Comoro na Mwenyekiti wa Bunge la Viongozi wa Nchi na Serikali wa AU Azali Assoumani, Bingwa wa AfCFTA na Rais wa Zamani wa Niger Issoufou Mahamadou, Katibu Mkuu wa AfCFTA Wamkele Mene, Mawaziri na makatibu Wakuu, sekta ya kibinafsi miongoni mwa wengine walihudhuria mkutano huo.
Tamati…