Katibu wa Kudumu katika Idara ya  Huduma za Magereza  Esther Ngero amejiuzulu.

Haya yanajiri wiki moja tu baada ya kuhamishwa kwake kutoka idara ya Utendaji na Usimamizi wa Huduma katika Ofisi ya Waziri  Mwenye Mamlaka  hadi Idara   Huduma za Magereza  iliyoko katika Wizara ya Usalama wa Ndani

Katika taarifa  kwa vyombo vya habari  Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei  amesema Ngero amejiuzulu kwa sababu za kibinafsi.

“Mkuu wa Nchi na Serikali amewasilisha shukrani zake kwa Bi Ngero kwa utumishi wake kwa taifa na kumtakia kila la kheri katika juhudi zake zote za siku zijazo,” Ujumbe wa Mkuu wa Utumishi wa Umma umearifu.

Koskei amesifia Ngero kama aliyekuwa kwenye mstaari wa mbele kubuni   mfumo wa kitaasisi ili kusaidia  wizara na idara mbalimbali kutekeleza wajibu wao.

“Katika muda wake ofisini, Bi Ngero amekuwa muhimu katika kuanzisha mfumo wa kitaasisi ili kusaidia utekelezaji wa majukumu ya Idara mbalimbali za serikali,” Koskei alisema.

Ngero alipelekwa katika idara ya Magereza katika mageuzi yaliyotekelezwa na rais William Ruto kufuatia sakata ya Ununuzi wa vyandarua iliyogubika Mmalaka ya KEMSA na kusababishwa kuwachishwa kazi kwa katibu wa Wizara ya afya Jospehine Mburu.

Katibu Mkuu wa Huduma ya Magereza Mary Muthoni aliteuliwa  kuchukua nafasi ya Mburu katika wizara ya Afya Ngero nae akichukua wadhfa wa Muthoni katika Idara ya Magereza.

Rais Ruto alimhamisha  Katibu wa Kudumu wa Huduma za Matibabu Peter Tum hadi Michezo.

Katibu wa Mifugo Harry Kimtai alichukua nafasi ya Tum katika Jumba la  Afya House huku  Ephantus Kimani wa Idara ya Misitu  akibadilishana nafasi na Gitonga Mugambi wa Umwagiliaji.