Mitihani ya kitaifa ya darasa la nane KCPE na gredi ya sita KPSEA imeanza rasmi hii leo kote nchini.

Hii leo wanafunzi wa darasa la nane watafanya somo la Hesabu kuanzia saa mbili asubuhi kabla ya kufanya mtihani wa Kiingereza saa tano unusu asubuhi na kisha insha ya Kiingereza saa nane unusu mchana.

Nao wanafunzi wa gredi ya sita ambao wanaofanya KPSEA kwa mara ya kwanza wanaanza na somo la Hesabu saa mbili unusu asubuhi na kisha Kiingereza saa tano asubuhi.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu anaongoza maafisa wa ngazi ya juu serikalini kufuatilia zoezi hilo katika maeneo mbalimbali kote nchini.

Akizungumza kutoka kaunti ya Mombasa asubuhi hii, waziri Machogu ametoa hakikisho kuwa mtihani huo hautafuja akisisitiza kua mikakati imewekwa kuzuia wizi wa mtihani.

“Mwaka huu tunatekeleza sera ya uwajibikaji wa kibinafsi.  Kila msimamizi wa kituo, msimamzi wa mtihani na walimu wakuu watatabeba mzigo wao wenyewe iwapo kutakua na ukiukaji wa sheria za mtihani,’’ alisema Machogu.

Mawaziri wengine na maafisa wa ngazi ya juu katika sekta ya Elimu wameongoza zoezi la ufunguzi wa shehena ya mitihani katika kaunti mbalimbali na wanatarajiwa kuzuru shule kukagua zoezi hilo.

Waziri wa michezo na Vijana Ababu Namwamba ameongoza ufunguzi wa shehena ya mtihani katika eneo bunge la Westlands jijini Nairobi, Waziri wa Maji Alice Wahome amesimamia zoezi hilo kaunti ya Muranga, huku mwenzake wa Uchimbaji Madini Salim Mvurya akishuhudia ufunguzi kaunti ya Kisumu.